John Nyanje
Kwanza nitumie abra hii kuwashukuru wahariri waandimizi wenzangu kwa kunipa fursa hii ajuadi inayonipahadhi ya kuandika makala haya ya kwanza ya jarida hili la kimtandao laUsuli. Kwa hakika, hii ni tajamala kubwa sana, kwani sina chochote cha ziada, isipokuwa raghba kama mwanazuoni wa maswala ya Jumuiya yetu pendwa ya Afrika Mashariki. Makala haya, ya Usuli yanapania kuangazia maswala ya sheria za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na taasisi zake.
Naonelea bora kufungua makala haya kwa kuandika kile ninachokiona kama kipengele cha kwanza cha "ilani tarajiwa" ya jarida hili. Ilani ndio mwongozo wa taasisi yoyote inapotarajia kulivulia njuga jambo lolote lile. Ndio maana wanasisasa hutupatia ilani zao kila mkondo wa siasa unapokaribia. Vilevile, wakomunisti walituandikia walivyotaka na jinsi ya kufanikisha matakwa hayo naye Mwalimu Nyerere akatupa azimio la Arusha kama ilani na muongozo kwetu.
Hivyo basi, nimeona niandike kupitia makala haya, kipengele cha kwanza cha kile ninachokiona kama ilani tarajiwa ya jarida hili la Usuli. Katika maisha yangu ya uanazuoni na uchapishaji, kuna mambo kadhaa yanayonitia nyongo na nisiyoyataka. Kama mhariri mwandamizi wa jarida hili, nataka kuyasema mambo haya kwa wote watakaochangia katika jarida hili na wale watakaokuwa wakiyasoma makala haya mara kwa mara.
Moja, sitaki kuyaandika makala haya kwa lugha ya Kiingereza inayotumika kila siku katika taasisi za Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki. Kama anavyosema Jenerali Ulimwengu, mwanasheria na mwanahabari aliyebobea, wasomi wengi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki hukibeza Kiswahili kama lugha ya kiwango cha pili, ya kutumiwa sokoni kubishania bei ya maharagwe, au kwenye majukwaa ya kisiasa kutamka porojo na uongo wa kuleta maendeleo. Anaendeleza kwa kusema kuwa Kiswahili kimefanywa kuwa lugha ya umbea, porojo na majibizano yasiyo na tija. Wengine kama mwanazuoni Profesa Chacha Nyaigoti-Chacha, mara nyingi huomboleza jinsi Kiswahili kinavyoborongwa, iwe katika hotuba za umma, redioni au kwenye runinga.
Mkataba wa uanzishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unatambua nafasi ya Kiswahili katika eneo hili na unaeleza kuwa Kiswahili kinakubalika na kuendelezwa kuwa lugha ya Jumuiya huku Kiingereza kikisalia kuwa lugha rasmi (Sekretarieti ya EAC, 1999). Katika kukuza ari ya utangamano, Jumuiya ilianzisha Tume ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, ambayo inashughulikia maendeleo na utafiti wa Kiswahili. Isitoshe, tarehe 25 Agosti, 2016, Bunge la Afrika Mashariki liliazimia kuwa Kiswahili kitambulishwe kuwa mojawapo ya lugha rasmi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hivyo, sitaki jarida hili liwe la kutokukienzi kiswahili kama mengine yaliyotangulia awali. Nataka wote watakaochapishwa katika makala haya ya Usuli wajisikie huru kujieleza katika lugha waipendayo hata kama ni lugha ya mama almuradi chimbuko lake ni Afrika. Kwa maoni yangu, iwapo jarida hili litataka kuwa na ushawishi mkubwa katika maswala ya usomi wa sheria na taasisi za Afrika Mashariki, lazima lijikite katika desturi flani. Desturi hii ni ile ya kukikuza, kukienzi na kukithamini Kiswahili.
Pili, sitaki jarida hili liwe na muonekano wa kuandikwa kupitia macho ya uanazuoni wa ughaibuni. Usomi, hasa wa sheria za kimataifa, umejikita katika ukoloni mamboleo. Wanazuoni wengi wanapoandika kuhusu taasisi za Afrika, huandika ili kuwafurahisha ama kujipendekeza katika hadhira za wasomi walio katika mataifa ya Ulaya na Marekani. Kama anavyoteta mwanazuoni ndugu Oumar Ba, utafiti huhusisha shughuli ya kuwavua nguo watu wengine ili waonekane uchi. Pia ni mchakato wa kushusha baadhi ya watu hadhi, waonekane viumbe vidogo: kuwaweka chini ya hadubini ili kuchungulia katika maisha yao ya faragha, siri, miiko, kufikiri, na malimwengu yao matakatifu. Hivyo basi inabidi katika utafiti na uandishi wetu kuhusu Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki tujiulize, je juhudi zetu za kujikomboa zinaeneza mahusiano ya ukoloni mamboleo? Je, ni kwa kiwango gani tunashiriki katika kuendeleza dhuluma, hasa kama watafiti wazawa wa Jumuiya yetu ya Afrika mashariki? Je, inamaanisha nini kupitisha ajenda ya utafiti dhidi ya ukandamizaji katika muktadha ambao maarifa yote yanaundwa na umoja wetu kama wanamajumui?
Hivyo, sitaki kuandika nadharia za Ulaya za kufananisha taasisi zetu kama vile mahakama ya haki Afrika Mashariki na mahakama ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. Nimechoka na hizi nadharia. Nataka nadhariaza kiafrika na za kizawa, ubuntu na kadhalika. Sitaki kuendelea na uhalifu huu wa kisomi wa udhalilishaji na uvuajinguo wa taasisi zetu za Jumuiya. Ndugu Apollin Koagne Zoupet anatukumbusha kwamba, katika enzi za kupigana dhidi ya ukoloni katika miaka ya sitini, mataifa ya Afrika yalifuata kile anachokiita 'haki za uanzilishaji'. Hii ni mojawapo ya nadharia sugu za Mwalimu Nyerere kuhusu uanzilishi wa mataifa mapya kwa kukataa kukubali viwango vya kimataifa vya kanuni ambazo hawakuchangia na ambazo, zimekuwa chombo cha uonevu kwao kupitia mataifa ya ughaibuni'. Hivyo ningependa kuona Usuli ikipigania nadharia hizi za kiafrika za usomi wa taasisi za sheria za kimataifa kama alivyofanya Mwalimu Nyerere.
Tatu, Sitaki pia kuandikiwa na watu wasiolelewa Afrika. Ndugu Oumar Ba, katika makala yake; Wazungu na Wamarekani hawajui Afrika: Tafsiri, ufafanuzi,na Ukusanyaji, anaeleza kuwa hatufai kuendelea kuwaachia "watu wa nje" kututafsiria, kutufafanulia na kutukusanyia takwimu zetu kuhusu taasisi zetu, sheria zetu na mifumo yetu. Hivyo, itabidi tujitathmini kwa kina sana kama anavyofanya mwanazuoni ndugu Profesa Dunia Zongwe, akieleza kuwa, endapo wanazuoni wa sheria za kimataifa Afrika wanataka kujibu wito wa wazi wa kuondoa ukoloni katika mtaala wa kisheria barani Afrika, lazima watafiti na wachapishe wao wenyewe. Vitabu vya sheria za Afrika kutoka mashirika makubwa ya uchapishaji katika nchi za Magharibi hujaa katika maktaba na madarasa ya vyuo vikuu jumuiyani kwetu na kwingineko barani Afrika, si kwa sababu nchi za Magharibi zilipanga njama dhidi ya Afrika. Bali, kwa kuakisi matokeo pungufu ya utafiti na uchapishaji wa kisayansi barani mwetu, wasomi wa sheria na taasisi za jumuiya kutoka Afrika hawaandiki kwa wingi unaostahili. Hivyo basi, ngoma zetu zinapopigwa hazilii kwa sauti kubwa na hazisikiki mbali, zinazama katika bahari ya zile za ughaibuni. Usuli ni mwanga mpya wa kurekebisha hili katika Jumuiya yetu. Wasomi wote, wadogo kwa wakubwa, chipukizi kwa waliobobea, wake kwa waume, matabaka yote, hasa wanaotoka katika Jumuiya yetu, nawasihi muitikie wito huu wa kuelezea hadithi zetu tutakavyo wenyewe katika Jumuiya yetu.
Nne, Sitaki kunyimwa uhuru wa kujieleza katika mazingira ya kiutafiti na kiusomi. Sitaki kabisa kuambiwa kwamba kuna mijadala ambayo jarida hili la kisomi haliwezi kuwa nayo kwasababu litawakera wengine, hasa watawala, wadini, na wafuasi wao, ama kundi lolote lile Almradi mijadala iwe ya heshima na hadhi, isiwe ya kubeza, kukejeli ama kukandamiza wengine. Usuli inapaswa kuchukua msimamo wa kujadili yote hayo katika taasisi za Jumuiya yetu ya Afrika mashariki. Hiki sio chombo cha wanazuoni tu, ni chombo cha kila raiya wa Afrika Mashariki. Kwangu, ni chombo cha ukombozi, ni mojawapo ya ukuzaji wa demokrasia yetu, kuelezea fikira zetu na kuhoji taasisi zetu pamoja na viongozi wake. Inabidi usuli iwe kiwanja cha uhuru wa mawazo, fitina lazima iwe mwiko kwetu, daima tuwe wakweli, na tusimamie ukweli wa midahalo kupitia mijadala hata kama hatuzikubali ama kuziunga mkono mada zenyewe.
Mwisho, Sitaki makala haya yatafsiriwe kwa lugha za kighaibuni kwa ajili ya kuchapishwa ila yanaweza kutafsiriwa kwa lugha zozote za kiafrika. Aliye na haja sana ya utafsiri akajifanyie mwenyewe. Natumai nimeweza kufanikisha lengo la kuieleza ilani tarajiwa ya usomi,utafiti na uandishi wa taasisi na sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa kuwa Usuli ndilo jarida la kwanza la kimtandao katika historia kuandaa sehemu ya kuelimisha na kubadilishana mawazo katika Jumuiya yetu kuhusu taasisi zetu na sheria zake, basi huu ndio mwongozo ambao ningependa kuona mhariri mkuu na sisi wahariri waandamizi tukiufuata. Hii ikawe chachu ya mabadiliko katika mtaala, kufundisha, kutafiti na kuchapisha kuhusu Jumuiya ya Afrika mashariki, taasisi zake na sheria zake. Naomba Usuli ijaaliwe Sada na Sudi katika kutimiza malengo haya muhimu. Daima idumu Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki.