Na Mheshimiwa Yusuf Shikanda*
Mioyo yetu imejaa huzuni, ewe Mola tufariji,
Huzuni ambayo ni ya kina, kisha ya kibinafsi,
Tumepata pigo la ghafla, pigo lenye uzani,
Majanja kasusia uzima, katuacha bila kwaheri,
Ama kweli Maisha kigeugeu, hatima yake mauti,
Buriani Gwiji Majanja, pumzika kwa amani.
Maisha yetu yatakuwa tupu, katika mambo alotuangazia,
Thamani yake ilionekana, katika kile alichotoa,
Alikua mkarimu wa kutoa, bila kujali alichopokea,
Amuhifadhi katika pepo, mwenye uwezo Rabana,
Buriani Gwiji Majanja, pumzika kwa amani.
Alikua mcheshi ajabu, na mwenye busara tajika,
Bila kujali uwezo wake, alikua na tabia ya upole,
Likua mjuzi wa sheria, kukuza sheria ya nchi,
Idara ya mahakama twalia, Mnara umeondoka,
Buriani Gwiji Majanja, pumzika kwa amani.
Mahakama itakukumbuka, ulijitolea kwa uchangamfu,
Kiongozi mwenye msukumo, mantiki katika fikira,
Ya Allah mpe Jannah, Majanja wetu kipenzi,
Buriani Gwiji Majanja, pumzika kwa amani.
Maisha ni kituo tu, sote tupo safarini,
Kwa wengine safari ni ya kasi, wengine ni polepole,
Na wakati safari inaisha, tutafanya hatua nzuri mbele,
Buriani Gwiji Majanja, pumzika kwa amani.
Nenda Gwiji nenda, kazi ya mola aijua Mola,
Na upate amani ya milele, kama tuzo letu maalum,
Akusamehe mapungufu yako, na atufariji tulobaki,
Buriani Gwiji Majanja, pumzika kwa amani.
* Yusuf Abdallah Shikanda ni Hakimu Mkuu anayehudumu katika Mahakama ya Shanzu, Mombasa, Kenya.